RAIS JAKAYA KIKWETE AIPONDA RIPOTI YA MAFURIKO MBELE YA MKUU WA MKOA JOEL BENDERA NA WATENDAJI WAKE KATIKA KIJIJI CHA MAGOLE KILICHOKUMBWA NA MAFURIKO MOROGORO.


Rais Jakaya Kikwete akiangalia moja ya nyumba zilizobomolewa na mvuailiyosababisha mafuriko wiki iliyopita katika Kijiji cha Mateteni, Dakawa, wilayani Kilosa alipotembelea maeneo hayo jana. Picha na Juma Mtanda.
 
MOROGORO
RAIS Jakaya Kikwete ameikataa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kuhusu waathirika wa mafuriko na waliokosa makazi na kumpa siku moja kukaa na timu yake kuandaa nyingine inayoendana na hali halisi ya janga hilo.


Eneo la Dumila, Morogoro lilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha wakazi wake kupoteza makazi na mali huku mamia ya magari yakiwamo mabasi yanayosafirisha abiria kukwama baada ya kubomoka kwa Daraja la Magole linalounganisha Barabara ya Dar es Salaam na Dodoma.

Mvua hizo zilizonyesha kwenye Wilaya ya Kilosa, ndizo zilisababisha kufurika kwa Mto Mkundi unaopita kwenye eneo hilo.

Taarifa ya Bendera

Bendera alitoa taarifa ya mafuriko kwa Rais Kikwete kwa niaba ya viongozi wa mkoa, wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa taasisi mbalimbali akisema wananchi 12,472 wamepoteza makazi. 


Alisema pia kuwa nyumba 1,141 zilibomoka na 2,551 ziliingiliwa na maji huku kaya 2,759 zikiathiriwa na mafuriko. Bendera alisema misaada ya mahema na vyakula imeanza kutolewa pamoja na dawa za kukabiliana milipuko ya magonjwa endapo itatokea.

Alisema pia kuwa tayari baadhi ya miundombinu imeanza kurejea kama kawaida huku huduma za majisafi zikitolewa na magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha Zimamoto Morogoro na Kampuni ya China ya High Quality Consulting and Development Solutions. Bendera alisema pia kuwa jumla ya Sh53.7milioni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya muda ya waathirika hao.

JK aikataa taarifa

Rais Kikwete aliyekuwa akikatizakatiza taarifa hiyo ya Bendera kwa maswali na ufafanuzi, alizikataa takwimu hizo akisema hazionyeshi uhalisia. Akizungumza na wananchi wa eneo hilo wakiwamo waliokuwa kwenye kambi iliyoko Sekondari ya Magole, Rais Kikwete aliwahakikishia upatikanaji wa vyakula, dawa na majisafi na salama.

Pia aliviagiza viwanda vya magodoro kuzisaidia haraka iwezekanavyo, familia zilizoathirika na kuahidi kuwa Serikali italipa baadaye ili kuwaepusha wakazi hao na hasa watoto na athari za kiafya.

Alisema kazi ya ujenzi wa makazi ya muda itafanywa JWTZ na si makandarasi kuepusha baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa mafuriko hayo. Rais Kikwete aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuangalia uwezekano wa kutoa magogo yaliyoziba katika makaravati na kuzibua mifereji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.

Akizungumzia ripoti hiyo Rais Kikwete alisema: “Mmeshindwa kufafanua watu walioathiriwa na mafuriko hayo ni wangapi na wanasaidiwa vipi hasa katika mahitaji mbalimbali na muhimu ya kimsingi kama chakula.

“Taarifa yenu inanitia shaka. Sasa ninawataka viongozi wa mkoa pamoja na Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote wa halmashauri kurudia upya kumbukumbu zenu na kupata idadi kamili ya waathirika ili kujua namna ya kuwasaidia. 


“Ninyi kama viongozi na mnashughulikia maisha ya watu, mnatakiwa kuwa na kumbukumbu zenye usahihi wa majina na kama hamna uhakika wa majina mnaomba vyakula kwa ajili ya nani? Misaada mingine kwa wahisani ya nini ?. HAMIDA SHARIFF-MWANANCHI.

0 Response to " RAIS JAKAYA KIKWETE AIPONDA RIPOTI YA MAFURIKO MBELE YA MKUU WA MKOA JOEL BENDERA NA WATENDAJI WAKE KATIKA KIJIJI CHA MAGOLE KILICHOKUMBWA NA MAFURIKO MOROGORO."

Post a Comment

wdcfawqafwef