Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi
la Polisi mkoani hapa limetoa wito kwa wananchi wa Mkoa huu kutumia
dhana ya Ulinzi jirani katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismas
inayotarajiwa kuanza rasmi kesho.
Wito
huo umetolewa leo asubuhi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas wakati alipokuwa
anaongea na waandishi wa habari kuelezea mikakati ya Jeshi hilo katika
kipindi hiki cha sikukuu.
Alisema
mara nyingi katika kusherehekea baadhi ya watu huwa wanakwenda kwenye
ibada na kutembelea maeneo mbalimbali huku wakiacha nyumba zao bila
waangalizi hali ambayo inaweza kusababisha uhalifu kutokea.
“Ni
vema kumuacha mtu nyumbani pindi wengine wanapokuwa kwenye ibada au
matembezi na pia kutaarifu majirani hali ambayo haitatoa mwanya kwa
wahalifu na huu ndio Ulinzi Jirani”. Alisisitiza Kamanda Sabas.
Aidha
Kamanda Sabas aliwataka watumiaji wa vyombo vya usafiri barabarani wawe
makini kwa kufuata sheria zote usalama barabarani na kuwataka
wasiendeshe vyombo hivyo wakiwa wamelewa, huku akiwataka watembea kwa
miguu wawe waangalifu na watoto wasitembee peke yao bali waambatane na
wakubwa.
Kwa
upande wa maeneo ya starehe aliwakumbusha wazazi wawe makini na Mabwawa
ya kuogelea (Swimming Pool) yaliyopo katika hotel mbalimbali kwani kuna
mengine yanakina kirefu hali ambayo inaweza kusababisha madhara kwa
watoto wao.
Kuhusu
kumbi za disko amewataka wamiliki wa maeneo hayo kutoruhusu idadi zaidi
ya wateja tofauti na uwezo wa kumbi zao na kuwaomba wananchi wa mkoa
huu watoe taarifa haraka mara baada kuona vitendo vya ukiukwaji wa
sheria vinatokea katika maeneo yao.
Hata
hivyo amesema Jeshi hilo limejipanga vizuri katika kudhibiti vitendo
vyovyote vya uhalifu si katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismas na
Mwaka Mpya bali wakati wote.
0 Response to "POLISI ARUSHA YAWAOMBA WANANCHI KUIMARISHA ULINZI JIRANI KIPINDI CHA SIKUKUU "
Post a Comment