Khadija Mngwai na Nicodemus Jonas
SHIRIKISHO
la Soka la Kimataifa (Fifa) limeipa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia
hadi Januari 27, kuanzia jana liwe limetoa maelezo ya uhakika kuhusiana
na usajili wa Emmanuel Okwi.
Usajili wa Okwi umezua utata mkubwa na kuzigonganisha timu nne kutoka katika nchi za Afrika Mashariki na Afrika Kaskazini.
Simba,
Yanga za Tanzania, SC Villa ya Uganda (zote kutoka Afrika Mashariki) na
Etoile ya Afrika Kaskazini, kila upande uko ndani ya mgogoro wa
mchezaji huyo mmoja.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema Fifa imetoa agizo hilo
huku ikisisitiza inataka kujua kuhusiana na malipo ya Mganda huyo kutoka
Simba kwenda Etoile.
Ikiwa ndiyo siku moja tu tangu Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya TFF kusitisha usajili wa Okwi Yanga, Rage amesema amepokea
ujumbe kutoka Fifa ambao unaitaka klabu hiyo ya Tunisia kutoa maelezo
hayo.
Simba inadai dola 300,000 (Sh milioni 480) ilizomuuza Okwi kwa Etoile na hadi leo imekuwa ‘ikiingia huku na kutokea kule.’
“Tumefarijika sana na taarifa hiyo, tunajua haki lazima itatendeka,
maana awali baadhi ya watu wa Simba waliamini kuwa nilikula fedha ya
Okwi,” alisema Rage.
Rage ndiye alihusika katika mauzo ya Okwi na
amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kufanya mchahato huo kwa njia ambayo
ingeipatia Simba fedha kwa wakati mwafaka.
Aliongeza kuwa, Simba haina shida na Okwi ila wanachohitaji ni malipo
yao na kudai kuwa walikubaliana atakapokuwa anauzwa, Simba itapata
mgawo wa asilimia 20 za usajili, hivyo anashangaa mpaka sasa anaichezea
Yanga, wakati wao Simba hawajapata mgawo wowote.
Gazeti hili
lilipomuuliza Katibu wa Yanga, Beno Njovu juu ya sakata la Okwi kuzuiwa
kuichezea timu yao, alisema: “Sisi pia tunasikia kupitia vyombo vya
habari, kama ni mchakato tulifanya kihalali, tuna uhakika na
tulichokifanya, tunasubiri barua rasmi kutoka TFF kisha tutatoa tamko.”
Aidha, Rage ametangaza mabadiliko katika sekretarieti ya Simba,
ambapo Ezekiel Kamwaga ameteuliwa kuwa katibu mkuu, akisaidiwa na
Stanley Phillip kama Katibu Msaidizi huku Asha Muhaji akiteuliwa kuwa
Ofisa Habari.
Wengine ni Eric Kiete (Mhasibu), Hussein Mzei (Ofisa Utawala), Amina
Kumwambe (Ofisa Utawala Msaidizi) na Issa Juma Matayo (Mwangalizi wa
Ofisi).
Saturday 25 January 2014
0 Response to "OKWI: FIFA YATOA SIKU TANO"
Post a Comment