PICHA|MAKTABA
Watu 10
wamefariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti
zilizotokea mikoa ya Pwani na Mwanza.Katika ajali ya mkoani Pwani, watu
saba wamefariki dunia na wengine tisa wakiwa majeruhi baada ya basi dogo
walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori huko Chalinze
Mzee, Barabara ya Chalinze - Segera wilayani Bagamoyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema jana kwamba ajali hiyo
ilitokea saa mbili usiku wa Machi 4 na kwamba watu hao tisa hali zao ni
mahututi.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Msata kwenda Dar es Salaam na lori ambalo lilikuwa likitokea Chalinze kwenda Tanga.
Aliwataja
waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Ismali Hussein, Ndege
Ally, Tunu Said, Khalfan Hussein, Tumaini Hussein, Jaffar Selemani na
Emmanuel David ambao miili yao ilihifadhiwa katika Kituo cha Afya
Chalinze.
Waliojeruhiwa
katika ajali hiyo ni kondakta wa basi hilo, Deo Moses, dereva wa lori,
Shaban Omar; utingo wa lori, Shoshy Mohamed na mwanafunzi darasa la
kwanza, Shule ya Msingi Kwaifugo Mkata, Abdul Wela. Wengine ni Bitela
Msuha, Zaina Mkombozi, Salumu Idd, Chadugu Paulo, Geofrey Anthony na
Juma Athuman. Majeruhi wengine majina yao hayakutambulika mara moja.
Alisema
majeruhi wengi wa ajali hiyo wameumia vibaya baadhi wamevunjika miguu na
mikono na wote walipelekwa Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu.
Kamanda Matei alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Hata
hivyo, mashuhuda wa ajali hiyo, Hussein Khalfani na Yusufu Hussein
walisema ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa basi hilo alipokuwa
akijaribu kuyapita malori waliyokuwa mbele yake.
Mwanza
Watu watatu wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kugonga daraja na kupinduka.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlohola alisema ajali hiyo ilitokea
jana saa 3:40 asubuhi katika Kijiji cha Ng’ombe wilayani Misungwi baada
ya tairi la nyuma upande wa kulia wa gari hilo lililokuwa likitokea
Mabuki kwenda Mwanza, kupasuka.
Alisema
dereva wa gari hilo, Patric Peter (28) alifariki dunia pamoja na abiria
wengine wawili, Makoye Nyanda (30) na Hawa Abel (25).
Aliwataja
majeruhi kuwa ni Angelina Abel (24), Shija Kabuki (22), Bune Chenya
(40) na Johari Malungu (24) ambao wote wamelazwa katika Hospital ya
Rufaa ya Bugando.
0 Response to "Ajali zaua 10 Mwanza, Chalinze "
Post a Comment